juzi niliona picha ya watoto wa kibongo wakiwa darasani (http://harakati.blogspot.com/). jambo la kusikitisha ni kuwa, inavyosemekana, mbunge wa sehemu hiyo ni mmoja kati ya waliootesha mizizi bungeni na mtu mwenye nafasi serikalini. lakini hakuna chochote alichokifanya hadi sasa. watu wake, ambao ndiyo waliomchagua na kuendelea kumchagua, hawaelewi lolote (na kama wanaelewa basi wanaogopa kusema). na si huyu mbunge tu, inasemekana kuna wengine walio na nafasi serikalini na kwingineko wanaotokea sehemu hiyo.
kama kweli huyu mbunge angekuwa alitaka nafasi ili alete maendeleo kwa watu wake, nini alichofanya miaka yote hii ya ubunge wake? na hii ni sehemu moja tu. nina uhakika hali hii ipo nchi nzima. ila kwingine bado hakujafichuliwa. sasa kama hawa viongozi si viongozi jina, basi ni nani? kwani kwa jinsi inavyoonekana hakuna lolote wanalolifanya kwa niaba ya wachovu. ni wazi wako bungeni, na kwenye nafasi nyingine, kama wanowamba ngoma tu. wanavutia upande wao. kama hali hii iko nchi nzima - na hakuna dalili za kuonyesha kuwa kuna tofauti kubwa sehemu nyingine - basi wanyalukolo watakoma ubishi. nchi iko na itabaki kwenye matope. kama gari inayozungusha magurudumu tu. haiendi popote. mabosi hawashuki kusukuma hata siku moja (ati suti ichafuke?).
niwazi kuwa watu fulani wananufaika zaidi ya wengine kwa jinsi hali ilivyo. na inavyoendelea kubaki hivyo ndiyo wanavyozidi kuvimbiwa. wakati wachovu wanazidi kufa kwa njaa na maradhi. dhahiri viongozi hawa hawaoni aibu wala kujisikia vibaya kwa kuwakandamiza ndugu zao. hali hii itaendelea mpaka lini?