kila nikiangalia pande mbali mbali za afrika, na hasa mijini, naona ubinadamu unazidi kupungua tu. watu hawawajali wenzao kama ilivokuwa enzi zile. vijijini ndiyo unaweza kuona bado watu wanaonyesha utu. ingawa nako kuna matatizo yake - elimu ya giza au mambo ya mazingara, kwa mfano, yako mbele sana. nachokiona kwa wingi ni ule uzungu wa kusema, "everybody for themselves and god for us all - kila mtu ajue lake mungu ndiyo wetu sote." huu ni usemi unaotia nguvu utengano. kwa hakika ni usemi wa kikabaila. ukabaila hushamiri kwa wachache wenye nguvu kuwakandamiza wengi wasio na kitu pia kuwanyima nafasi ya kujitoa kwenye kibano.
wakati nchi za kiafrika zinazidi kuwa fukara, kwa kukamuliwa na wababe wa kimarekani na wazungu wengine, viongozi wa kiafrika (vikaragosi wao) wanatuna wakati wananchi wao wanazidi kukondeana kwa umaskini. wakati huo huo nchi hizi hizi, zijulikanazo kama maskini kupita zote duniani (wakati viongozi wao ni kati ya matajiri kupita wote duniani), zina machimbo ya almasi, dhahabu n.k. ambayo huwatajirisha mabwanyenye wa kiyahudi, kiarabu na wazungu pasipo mfano. isingekuwa watu kama kina mobutu na wengineo wenye akili za kushikiwa kama yeye, waafrika wangeumia lakini si kiasi hicho. na isitoshe siyo kuumizwa na ndugu zao. kwa bahati mbaya viongozi wengi wa kiafrika wanataka wawe kama mobutu.
kwa mfano kulikuwa na habari kuwa raisi wa zamani wa tanganyika alinunua ndege ya kujirusha mwenyewe pale anapojisikia. wakati huo huo hospitali za serikali hakuna dawa (hospitali za kibinafsi hata kwenye ndoto haziingiliki). sitoshangaa kusikia wabongo wamekopa msemo wa wamarekani: maskini hawaumwi wanakufa.
wengine wanajidai kuvutia utandawizi kwa kukaribisha wawekezaji. tushawashitukia, janja yao tumeiona tangu juzi. ndo maana ukisema sana wanakukata kilimi. kwa bahati mbaya wengi wetu bado mabozo, wananunuliwa kirahisi kwa tv kubwa na mikweche ya riko (reconditioned automobiles) toka uarabuni na nchi kupe nyingine.
hala hala kesho kuna moto wajameni.
No comments:
Post a Comment